Wednesday 6 June 2012

                                                                                                           Leo, Juni  2012
Nisamehe

Mpole sina afia, sina nguvu za mwilini,
Kama mtoto nalia, nina uchungu moyoni,
Kujuta ninajutia, nimekuudhi fulani,
Dada nipe msamaha, ili nipate amani.

Nashukuru sikufuru, Mola asinadhibu,
Ingawa nilikudhuru, najua utanitibu,
Kwako nitapata nuru, nikisogea karibu,
Dada nipe msamaha, ili nipate amani.

Ili niwe na amani, msamaha ni muhimu,
Siwa mkosa imani, najua kuna hukumu,
Nahofu moto jamani, nisamehe nihitimu,
Dada nipe msamaha, ili nipate amani.

Uandishi kazi yangu, dada haina mipaka,
Nawafaa wa kiungu, nao waliopotoka,
Napoza wenye uchungu, nachafua wanotaka,
Dada nipe msamaha, ili nipate amani.

Donge nililokupa, kumbe si saizi yako,
Nashukuru ulitupa, lingenyonga koo lako,
Kama nyama ya mfupa, bila meno ni unoko,
Dada nipe msamaha, ili nipate amani.

Hatimaye nakuaga, ni mwishoni mwa shairi,
Nenda bafuni kukoga, unitoke uhinziri,
Sitaki tena kuzuga, sio mzuri ushari,
Achieng’ nisamehe, ili nipate amani.

Wasalaam.
Malenga Kiroboto Mpole, (Kimpole)
Itigo, Eldoret.