Saturday 16 November 2013

Our courses are custom-designed for all. You can even learn online if you are able to access the internet. Well, it's time you registered and got started!! Welcome.

Saturday 28 September 2013

Page 1 of Mswahili Newsletter

Mswahili huandaliwa na kutolewa kila Ijumaa na SAFARI GROUP
Nakala hii ya kielektroniki hutolewa bila malipo.

Saturday 4 May 2013

Wajinga wengi jamani


Mpole nimo chumbani, natunga nyingine tungo,
Namkosoa fulani, mwenye kusema uongo,
Vipi awe ukwelingi, hali amekuwa chongo,
Wengi wajinga jamani, wana radhi la ubishi.

Wana radhi la ubishi, wakianza hawasiti,
Mambo yao hayaishi, wanayo yenye risiti,
Kama kweli huwapishi, utaingia mashiti,
Wengi wajinga jamani, jepushe nao kiumbe.

Jepushe nao kiumbe, maisha haya mafupi,
Kama wataka utambe, utafumwa kwa rawapi,
Kesha kimya usiambe, kuamba kuna ukopi,
Wengi wajinga jamani, leo waitwa werevu.

Siddi Kiroboto Mpole

Kama kusoma mama


Nasema nao wadama, mawakili wa kusoma,
Wanaosema daima, kusoma ni kwa lazima,
Nipeni bila kukoma, sababu zinowatuma,
Kama kusoma ni mama, nambie baba ni nani?

Nambie baba ni nani, tena jina lake lipi,
Ndipo none tumaini, la sivyo sifa sikupi,
Bila kusoma jamani, wengi wanazila pipi,
Kama kusoma ni mama, nambie baba ni nani?

Mama huzaa hakika, akalea na kuasa,
Bali baba atakika, kunapojiri mikasa,
Basi wenzi nawataka, baba pewe ukurasa,
Kama kusaoma ni mama, nipe babna nifaulu.

Nipe baba nifaulu, kitabu sio mkate,
Nenda hata kwa hikalu, wahubiri nwakute,
Siketi nigeke mbulu, kamili wapi nipate,
Sawa kusoma ni mama, baba njoo unitunge. 


Malenga Sidi Kiroboto Mpole
Eldoret.

Thursday 17 January 2013

Umangati wengia kidedeani!!!

Mzee nimebaini, wana wanaofanana,
Hawatiki tofutini, wana mfanano wana,
Hawaji tena mjini, maswala kuchanjiana,
Umangati nauona, wangia kidedeani.

Acha nikwelezeni, hali zino mzelewe,
Umangati huno nini, na kidedea mjuwe,
Kinipata makosani, niteteni nisiwawe,
Umangati nauona, wangia kidedeani.

Nakumbuka utotoni, nilipokuwa na meno,
Nikiwa kwetu nyumbani, kwa baba na mama Chano,
Nikifundwa ya ujani, nilona haya maono,
Umangati nauona, wangia kidedeani.

Nilifundwa umangati, na mama pia na aba,
Si wema niwe sifwati, katika la siku saba,
Kwani huakupi cheti, kichora itesha raba,
Umangati nauona, wangia kidedeani.

Umangati huahidi, ahadi zilo kamili,
Huapisha ikibidi, ja wa Kwale Mswahili,
Lakini ngoma kurudi, ahadi kuitimili,

Umangati nauona, wangia kidedeani.
Kisha kuna kidedea, nifundishwa na wavyele,
Hiki cheza kuelea, na hurowa kwa utele,
Walinomba kwendelea, kizingatia milele,
Umangati nauona, wangia kidedeani.

Eti kina kumanisha, wazaaji walinena,
Halafu nisha wazisha, wankwisha ozeana,
Leo nona cha kutisha, kidea kina mikuna,
Umangati nauona, wangia kidedeani.

Ino mikuna naona, ni ile ya kimangati,
Ndo mana wazi nanena, kimengia umangati,
Vipi ikawezekana, kushangaa miye sati,
Umangati nauona, wangia kidedeani!!


Siddi Kiroboto Mpole
Mzee Kimpole”
Kimpola Language School,
Eldoret.

Tuesday 18 September 2012

Wanga wawa dume gani?!

Eddi nipelo sikizi, Mpole nasema nawe,
Umegeuka kilizi, sababu nomba nijuwe,
Una nini siku hizi, tuambie tukijuwe,
Wanga wawa dume gani, kulialia ja mwana.

Kulialia ja mwana, redioni gazetini,
Kifo nani hataona, ndo kijaze mdomoni,
Unawapotosha wana, toa mfano mwanani,
Wanga wawa dume gani, Mpole nakushangaa.

Mpole nakushangaa, malenga wa Visramu,
Kijua umekomaa, kumbe bado kuhitimu,
Ni bora ukinyamaa, usidhaniwe wazimu,
Wanga wawa dume gani, nahurumia mkeo.

Nahurumia mkeo, kwani kulea hakomi,
Hamna aso upeo, acha kuzitoa kemi,
Hujui kifo ni cheo, sio cha mapeni kumi,
Wanga wawa dume gani, wawasiwasika bure.

Wawasiwasika bure, hakuna anokwandama,
Zikumbuke hamrere, kwa wengi ulizotuma,
Ndizo zafanya uhare, pole hutaki kusema,
Wanga wawa dume gani, wanishangaza Mpole,

Wanishangaza Mpole, mie mkongwe bondeni,
Wazileta siku zile, Kizere kivuma ndani,
Uje kwangu tuselele, juma zima mafunzoni,
Wanga wawa dume gani, kulia achia wana.

Chombo kikitia nanga


Mzee ni ukumbini, na tabu la ujanani,
Natia macho miwani, nimsomee Fulani,
Maisha ya duniani, wangi hawajui nini,
Chombo kikitia nanga, si mwisho wa usafiri.

Si mwisho wa usafiri, hata kama umefika,
Huishi kwenye bandari, kwenda zaidi tataka,
Ipe mgongo bahari, na uikabili njia,
Chombo kikitia nanga, teremka kwa makini.

Teremka kwa makini, uikague sehemu,
Jua lengo kuu nini, nakili kwa tarakimu,
Kama ndipo ubaini, lau sipo ufahamu,
Chombo kikitia nanga, yasubiri maelezo.

Yasubiri maelezo, usanze bure kuranda,
Yako kote matatizo, kokote unakokwenda,
Hayakeri maulizo, wangi mno mewalinda,
Chombo kikitia nanga, usanze kutoa mali.

Usanze kutoa mali, itatwaliwa haraka,
Ufikiri mara mbili, uhakiki umefika,
Wanolipuuza hili, huchekwa wanapotoka,
Chombo kkitia nanga, sikiza yao wazee.

Sikiza yao wazee, kama miye Kimpole,
Tukiteswa tutetee, radhi tulinazo tele,
Acha nende waombee, Mola awone milele,
Chombo kikitia nanga, umkumbuke Rabuka.