Tuesday 18 September 2012

Wanga wawa dume gani?!

Eddi nipelo sikizi, Mpole nasema nawe,
Umegeuka kilizi, sababu nomba nijuwe,
Una nini siku hizi, tuambie tukijuwe,
Wanga wawa dume gani, kulialia ja mwana.

Kulialia ja mwana, redioni gazetini,
Kifo nani hataona, ndo kijaze mdomoni,
Unawapotosha wana, toa mfano mwanani,
Wanga wawa dume gani, Mpole nakushangaa.

Mpole nakushangaa, malenga wa Visramu,
Kijua umekomaa, kumbe bado kuhitimu,
Ni bora ukinyamaa, usidhaniwe wazimu,
Wanga wawa dume gani, nahurumia mkeo.

Nahurumia mkeo, kwani kulea hakomi,
Hamna aso upeo, acha kuzitoa kemi,
Hujui kifo ni cheo, sio cha mapeni kumi,
Wanga wawa dume gani, wawasiwasika bure.

Wawasiwasika bure, hakuna anokwandama,
Zikumbuke hamrere, kwa wengi ulizotuma,
Ndizo zafanya uhare, pole hutaki kusema,
Wanga wawa dume gani, wanishangaza Mpole,

Wanishangaza Mpole, mie mkongwe bondeni,
Wazileta siku zile, Kizere kivuma ndani,
Uje kwangu tuselele, juma zima mafunzoni,
Wanga wawa dume gani, kulia achia wana.

Chombo kikitia nanga


Mzee ni ukumbini, na tabu la ujanani,
Natia macho miwani, nimsomee Fulani,
Maisha ya duniani, wangi hawajui nini,
Chombo kikitia nanga, si mwisho wa usafiri.

Si mwisho wa usafiri, hata kama umefika,
Huishi kwenye bandari, kwenda zaidi tataka,
Ipe mgongo bahari, na uikabili njia,
Chombo kikitia nanga, teremka kwa makini.

Teremka kwa makini, uikague sehemu,
Jua lengo kuu nini, nakili kwa tarakimu,
Kama ndipo ubaini, lau sipo ufahamu,
Chombo kikitia nanga, yasubiri maelezo.

Yasubiri maelezo, usanze bure kuranda,
Yako kote matatizo, kokote unakokwenda,
Hayakeri maulizo, wangi mno mewalinda,
Chombo kikitia nanga, usanze kutoa mali.

Usanze kutoa mali, itatwaliwa haraka,
Ufikiri mara mbili, uhakiki umefika,
Wanolipuuza hili, huchekwa wanapotoka,
Chombo kkitia nanga, sikiza yao wazee.

Sikiza yao wazee, kama miye Kimpole,
Tukiteswa tutetee, radhi tulinazo tele,
Acha nende waombee, Mola awone milele,
Chombo kikitia nanga, umkumbuke Rabuka.