Friday 11 May 2012


Kilio cha Boda boda

Habari za kuzubaa, nyie mlio vitini,
Taratabu twatambaa, tukijia mlikoni,
Katu hatutabung’aa, tuishie kafarani,
Tuk-tuk zimwi kweli, limetumwagia unga,

Limetumwagia unga, na kutubwaga njaani,
Taratibu tunakonga, jamaa tulishieni,
Sie twaliita janga, bora katuloleeni,
Tuk-tuk zimwi kweli, limetumwagia unga,

Kheri lende majijini, litoke huku shambani,
Sasa kazi hatuoni, bukrata ashiyani,
Ushuru tulipieni, kiwa pato hatuoni,
Tuk-tuk zimwi kweli, limetumwagia unga,

Sio siri tunalia, hasa huku Magharibi,
Katu hatutatulia, twaja hata Nairobi,
Tutaja jiamulia, kipuza yetu maombi,
Tuk-tuk zimwi kweli, limetumwagia unga,

Japo ni njia ya pato, ni uhaini mkuu,
Ni kipato cha mkato, kwa idadi iso kuu,
Ndo twasihi Kiroboto, awasilishe kukuu,
Tuk-tuk zimwi kweli, limetumwagia unga,

Kwa ufupi viongozi, shoti tendeni khisani,
Tuondolee vigunzi, twendelee kwa amani,
Litende jijini kazi, lituachie shambani,
Tuk-tuk zimwi kweli, limetumwagia unga.

Hapa Kiroboto nilikuwa nawatetea wahudumu wa Boda Boda dhidi ya mjo wa tuk-tuk. Haa, nalo lilichapishwa kwenye Taifa Leo na kulumbwa na wengi hususan Malenga Wa Kijiweni, Abubakari Rajabu wa pale Steji Mjini mumias. Ni mwendeshaji Tuk Tuk na hivyo basi sikubungaa kuona akikinza! Ni rafiki yangu na asili ya lakabu yangu. nampenda! Mgalla umwuuwapo haki mpe jamani!!!
 

Wednesday 9 May 2012

Fundo chunga la Moyoni

Ewe unosoma lino, niwe mie nakujia,
Nakunyoshea mikono, magoti nakupigia,
Uneleze ya uono, ya wengi kuwachukia,
Fundo chungu la moyoni, linakufaidi nini.

Mbona wayatoa macho, mithili ya bundi kaka,
Na pia kisucho hicho, alani mbona siweke,
Eti mabezo kitocho, daima kasawijika,
Fundo chungu la moyoni, linakufaidi nini.

Kila mara kiniona, watamani kunifyanda,
Hata tunapokutana, kusalimu hutapenda,
Japo ni wa kwenu mwana, unapanga kuniponda,
Fundo chungu la moyoni, linakufaidi nini.

Ama kweli u zandiki, kanisani u shabiki,
Wajitia kushiriki, kutekeleza hutaki,
Maadaili wadhihaki, hata bora sishiriki,
Fundo chungu la moyoni, linakufaidi nini.

Iwapo mie tajiri, huji nikakupe siri,
Wapangia usihiri, wapanga kunihasiri,
Mwisho utie kaburi, kidhani metenda heri,
Fundo chungu la moyoni, linakufaidi nini.

Kwa ufupi ndugu zangu, tuasi yetu khiana,
Tusoneane machungu, ili tuweze kupona,
Chunga tusichushe Mungu, kwa daima kukinzana,
Fundo chungu la moyoni, linakufaidi nini.

Maelezo: Shairi hili nililitunga mwaka 2007 . Nilikuwa katika harakati za kujiunga na chuo kikuuu. Pia ni wakati huu ambapo mashairi yangu yalikuwa yakivuma mno katika gazeti la Taifa Leo. Si wengi waliokuwa wakifurahishwa na maendeleo yale. Ndiposa nikawasihi wayafundukhule mafundo nyoyoni kwani kila mja na nyota yake!!

Mnara wa walotuuka

Mwaambaje mashabiki, mpendao penye haki,
Mnopenda kudhihaki, mipigo ya kimziki,
Leo ninawahakiki, nitawapa yangu jeki,
Mnara wa lotuuka, mbona haurekebiki.

Sisemi ninadhihaki, miye ni kindakindaki,
Pia naipenda haki, na mwenye chuki kwa chuki,
Iwapo meinywa siki, mwambe nitie breki,
Mnara wa lotuuka, mbona haurekebiki.

Ikiwepo taharuki, hiyo yangu mabruki,
Bora nipige mswaki, kinywa kisizue chuki,
Nilipolenga mkuki, ni pa Kiswahili hiki,
Mnara wa lotuuka, mbona haurekebiki.

Nimeumwa kwa mawiki, kwa walosema ashiki,
Semi hazirekebiki, na mithali mahuluki,
Sasa swali washiriki, nijibu kimantiki,
Mnara wa lotuuka, mbona haurekebiki.

Mbona haurekebiki, mnara uso wa haki,
Sarufi haitiiki, bado mwasema si baki,
Ama mbovu mwadiriki, sumu hamnusuriki,
Mnara wa lotuuka, mbona haurekebiki.

Wengi wenu nahakiki, mmejitanda kaniki,
Mwatafuta na mikuki, m’ue Kiroboto hiki,
Ila mie sitishiki, kwani haizami haki,
Mnara wa lotuuka, mbona haurekebiki.

Nikiaga mashabiki, salamani mkabaki,
Mbakiapo rafiki, Mola na awabariki,
Nodhani ni unafiki, kishairi dai haki,
Mnara wa lotuuka, mbona haurekebiki.

Maelezo: Shairi hili nililitunga mwaka 2007 wakati ambapo mabadiliko mengi yalikuwa yakifanyiwa lugha ya Kiswahili hususan yakiongozwa na mwalimu Wallah Bin Wallah. Japo simpingi mwaliumu Yule, yapo mengi ambayo sikubaliani nayo kulingana na shairi langu hilo.

Tuesday 8 May 2012

Karibuni wapenzi washairi

Karibuni
Hatimaye nimetua,
Paso jua wala mvua,
Si kwamba nilipajua,
Ni Mola mwenye kwamua.

Karibuni mpate tungo za kimpole, tungo zangu mie tangu nilipojibwaga utunzini. Mola mwema awabariki mnapozisoma nudumu za humu.