Mnara wa walotuuka
Mwaambaje mashabiki,
mpendao penye haki,
Mnopenda kudhihaki,
mipigo ya kimziki,
Leo ninawahakiki,
nitawapa yangu jeki,
Mnara wa lotuuka, mbona
haurekebiki.
Sisemi ninadhihaki, miye
ni kindakindaki,
Pia naipenda haki, na
mwenye chuki kwa chuki,
Iwapo meinywa siki,
mwambe nitie breki,
Mnara wa lotuuka, mbona
haurekebiki.
Ikiwepo taharuki, hiyo
yangu mabruki,
Bora nipige mswaki,
kinywa kisizue chuki,
Nilipolenga mkuki, ni pa
Kiswahili hiki,
Mnara wa lotuuka, mbona
haurekebiki.
Nimeumwa kwa mawiki, kwa
walosema ashiki,
Semi hazirekebiki, na
mithali mahuluki,
Sasa swali washiriki,
nijibu kimantiki,
Mnara wa lotuuka, mbona
haurekebiki.
Mbona haurekebiki, mnara
uso wa haki,
Sarufi haitiiki, bado
mwasema si baki,
Ama mbovu mwadiriki, sumu
hamnusuriki,
Mnara wa lotuuka, mbona
haurekebiki.
Wengi wenu nahakiki,
mmejitanda kaniki,
Mwatafuta na mikuki, m’ue
Kiroboto hiki,
Ila mie sitishiki, kwani
haizami haki,
Mnara wa lotuuka, mbona
haurekebiki.
Nikiaga mashabiki,
salamani mkabaki,
Mbakiapo rafiki, Mola na
awabariki,
Nodhani ni unafiki,
kishairi dai haki,
Mnara wa lotuuka, mbona
haurekebiki.
Maelezo: Shairi hili
nililitunga mwaka 2007 wakati ambapo mabadiliko mengi yalikuwa
yakifanyiwa lugha ya Kiswahili hususan yakiongozwa na mwalimu Wallah
Bin Wallah. Japo simpingi mwaliumu Yule, yapo mengi ambayo
sikubaliani nayo kulingana na shairi langu hilo.
No comments:
Post a Comment