Fundo chunga la Moyoni
Ewe unosoma lino, niwe
mie nakujia,
Nakunyoshea mikono,
magoti nakupigia,
Uneleze ya uono, ya wengi
kuwachukia,
Fundo chungu la moyoni,
linakufaidi nini.
Mbona wayatoa macho,
mithili ya bundi kaka,
Na pia kisucho hicho,
alani mbona siweke,
Eti mabezo kitocho, daima
kasawijika,
Fundo chungu la moyoni,
linakufaidi nini.
Kila mara kiniona,
watamani kunifyanda,
Hata tunapokutana,
kusalimu hutapenda,
Japo ni wa kwenu mwana,
unapanga kuniponda,
Fundo chungu la moyoni,
linakufaidi nini.
Ama kweli u zandiki,
kanisani u shabiki,
Wajitia kushiriki,
kutekeleza hutaki,
Maadaili wadhihaki, hata
bora sishiriki,
Fundo chungu la moyoni,
linakufaidi nini.
Iwapo mie tajiri, huji
nikakupe siri,
Wapangia usihiri, wapanga
kunihasiri,
Mwisho utie kaburi,
kidhani metenda heri,
Fundo chungu la moyoni,
linakufaidi nini.
Kwa ufupi ndugu zangu,
tuasi yetu khiana,
Tusoneane machungu, ili
tuweze kupona,
Chunga tusichushe Mungu,
kwa daima kukinzana,
Fundo chungu la moyoni,
linakufaidi nini.
Maelezo: Shairi hili
nililitunga mwaka 2007 . Nilikuwa katika harakati za kujiunga na chuo
kikuuu. Pia ni wakati huu ambapo mashairi yangu yalikuwa yakivuma mno
katika gazeti la Taifa Leo. Si wengi waliokuwa wakifurahishwa na
maendeleo yale. Ndiposa nikawasihi wayafundukhule mafundo nyoyoni
kwani kila mja na nyota yake!!
No comments:
Post a Comment