Tuesday 17 July 2012

Mbogholi akoga

Mbogholi ni malaika?!

Mkwiro naukamata, kigoma nanzekipiga,
Mati natakaziita, zone Mbogoli kikoga,
Huyu mtoka Taveta, uungu akauiga,
Mbogholi ni Malaika, waja awona shetani.

Waja awona shetani, hasa wale wa siasa,
Amewatia doani, eti ni hakimu sasa,
Natakajua ni nani, Ludo amemtakasa,
Mbogholi ni Malaika, adharau viongozi.

Adharau viongozi, akawaita mikia,
Eti kikaza maozi, awaona masinia,
Naona akosa kazi, wengine kawangilia,
Mbogholi ni Malaika, wasoye mauzauza.

Wasoye mauzauza, wanasiasa asema,

Awaita walooza, kwa makali awachoma,

Kwamba wanajidekeza, wote atakawatema,
Mbogholi ni Malaika, ndiye aliyetimia.

Ndiye aliyetimia, kama siasa ajua,
Nani amemuambia, kina suluhu kifua,
Mpole namuusia, pae kijuwa kutua,
Mbogholi ni Malaika, kesho aende mbinguni.

Kesho aende mbinguni, kusiko hawa majibwa,
Ajuwe hayezekani, dunia iso na chapwa,
Siasa daima duni, ni kunguru alorembwa,
Mbogholi ni Malaika, Mpole namshangaa!

SYLVESTER OCHIENG
AlmaarufuKiroboto Mpole
Kituo cha Lugha za Ughaibuni,
Eldoret.

Tungo Mseto


Toloi kupata wana

Mpole ninaingia, na hongera chekwachekwa,
Nampongeza Rukia, Waluhya tunamjuwa,
Mola amemjibia, kwani wana amepewa,
Toloi kupata wana, ni ishara yake Mungu.

Ni ishara yake Mungu, Bwana wa wokovu wetu,
Tumpe yetu machungu, anaweza vyote vitu,
Mwenye dunia na mbingu, alomkumbuka Lutu,
Toloi kupata wana, kuimarishe imani.

Kuimarishe imani, kati yetu waumini,
Tutambue Mungu nani, tudumu kumuamini,
Siyumbeyumbe jamani, wala simjaribuni,
Toloi kupata wana, kweli ni mwamko mpya.

Kweli ni mwamko mpya, tulioupata waja,
Liwe ni fundisho Kenya, kuwa maombi daraja,
Bwana Mungu wa Eliya, tatupa tukimngoja,
Toloi kupata wana, ni furaha kwetu sote.

Ni furaha kwetu sote, tunamtukuza Mola,
Mungu Muweza wa yote, asante kujibu sala,
Tuzuie tusikwate, wewe huna kibadala,
Toloi kupata wana, ni hidaya kubwa hino,

Ni hidaya kubwa hino, Kiroboto naswifia,
Namwinua Mungu mno, tena namsujudia,
Katimizia maono, wale nilohurumia,
Toloi kupata wana, la ziada sina tena.

La ziada sina tena, ila nasaha hatima,
Toloi leeni wana, kwa ndia iliyo njema,
Wakamheshimu Bwana, isiwapate nakama,
Toloi kupata wana, shangwe Mulembe Ef Emu.

Ochieng’ O. Sylvester
Kiroboto Mpole”
Chuo Kikuu Cha Moi
Chepkoilel.






Kwaheri Mrono

Mpole nina kilio, kilio cha Kiswahili,
Silipati kimbilio, kulitia pigo hi9li,
Mauti faradhi ndio, bali hiki kikatili,
Kwaheri ndugu Mrono, mwalimu wa heba kubwa.

Twamshukuru Rabuka, kwa maishayo mwandani,
Sie tutakukumbuka, kwa kaziyo vitabuni,
Kukupeza ni hakika, sautiyo redioni,
Kwaheri ndugu Mrono, mwalimu wa heba kubwa.

Wapenzi wa Kiswahili, tumebaki vinywa wazi,
Kote metulia tuli, tangu lizame jahazi,
Mwenzetu kwa kwenda mbali, umetutia duwazi,
Kwaheri ndugu Mrono, mwalimu wa heba kubwa.

Bahari yetu si shwari, imechafuka watani,
Tangu uwe mhajiri, hatwoni chako kifani,
Twafazaika twakiri, hatutaki kuamini,
Kwaheri ndugu Mrono, mwalimu wa heba kubwa.

Kaketu wende salama, mikono yetu twapunga,
Wasalimie wa zama, akina Mwalimu Mbega,
Twakwombea kwa Karima, na dhiki atakutenga,
Kwaheri ndugu Mrono, mwalimu wa heba kubwa.

Kituoni nikifika, rambirambi nazituma,
Makiwa ndu’ watukuka, nayo familia nzima,
Haya mambo ya Rabuka, nayo mauko lazima,
Kwaheri ndugu Mrono, mwalimu wa heba kubwa.

Ochieng’ O. Sylvester
Kiroboto Mpole”
Chuo Kikuu Cha Moi
Chepkoilel.



Saturday 7 July 2012

Wangu lia shambani

Mpole nimeghasiwa, na waibaji wa miwa,
Nawamiminia dawa, sina shaka wauguwa,
Taksiri niwatowa, si kwa nia kuumbuwa,
Wangu ulie shambani, sondoke nao kiumbe.

Ungaingia shambani, una uhuru mwandani,
Chaguwa pahala ndani, utapotulia chini,
Hata kama mafichoni, sijali sitokuhini,
Wangu ulie shambani, sondoke nao kiumbe.

Uubambue maganda, ubakiye utakavyo,
Utende utavyotenda, upate wako mchovyo,
Kama mcheza kandanda, shinda jinsi uwezavyo,
Wangu ulie shambani, sondoke nao kiumbe.

Tafuna kisha unyonye, utamu saizi yako,
Mie nani nikukanye, shambani sina uchoko,
Maliza chafu usanye, na uende uendako,
Wangu ulie shambani, sondoke nao kiumbe.

Lakini nakwonya wewe, mzoea kugurisha,
Ya kwangu usiondowe, ukangia kuharisha,
La sivyo nikuripuwe, kufisha nitakufisha,
Wangu ulie shambani, sondoke nao kiumbe.

Kabula nitie tuo, mwenye kono ujitenge,
Nikupa langu funguo, na mwako pia sifunge,
Nikija nile chaguo, lolote usinipinge,
Wangu ulie shambani, sondoke nao kiumbe.

Utunzi wa: Malenga Kimpole,
Eldoret (K).