Saturday 7 July 2012

Wangu lia shambani

Mpole nimeghasiwa, na waibaji wa miwa,
Nawamiminia dawa, sina shaka wauguwa,
Taksiri niwatowa, si kwa nia kuumbuwa,
Wangu ulie shambani, sondoke nao kiumbe.

Ungaingia shambani, una uhuru mwandani,
Chaguwa pahala ndani, utapotulia chini,
Hata kama mafichoni, sijali sitokuhini,
Wangu ulie shambani, sondoke nao kiumbe.

Uubambue maganda, ubakiye utakavyo,
Utende utavyotenda, upate wako mchovyo,
Kama mcheza kandanda, shinda jinsi uwezavyo,
Wangu ulie shambani, sondoke nao kiumbe.

Tafuna kisha unyonye, utamu saizi yako,
Mie nani nikukanye, shambani sina uchoko,
Maliza chafu usanye, na uende uendako,
Wangu ulie shambani, sondoke nao kiumbe.

Lakini nakwonya wewe, mzoea kugurisha,
Ya kwangu usiondowe, ukangia kuharisha,
La sivyo nikuripuwe, kufisha nitakufisha,
Wangu ulie shambani, sondoke nao kiumbe.

Kabula nitie tuo, mwenye kono ujitenge,
Nikupa langu funguo, na mwako pia sifunge,
Nikija nile chaguo, lolote usinipinge,
Wangu ulie shambani, sondoke nao kiumbe.

Utunzi wa: Malenga Kimpole,
Eldoret (K).

1 comment: