Tuesday 17 July 2012

Tungo Mseto


Toloi kupata wana

Mpole ninaingia, na hongera chekwachekwa,
Nampongeza Rukia, Waluhya tunamjuwa,
Mola amemjibia, kwani wana amepewa,
Toloi kupata wana, ni ishara yake Mungu.

Ni ishara yake Mungu, Bwana wa wokovu wetu,
Tumpe yetu machungu, anaweza vyote vitu,
Mwenye dunia na mbingu, alomkumbuka Lutu,
Toloi kupata wana, kuimarishe imani.

Kuimarishe imani, kati yetu waumini,
Tutambue Mungu nani, tudumu kumuamini,
Siyumbeyumbe jamani, wala simjaribuni,
Toloi kupata wana, kweli ni mwamko mpya.

Kweli ni mwamko mpya, tulioupata waja,
Liwe ni fundisho Kenya, kuwa maombi daraja,
Bwana Mungu wa Eliya, tatupa tukimngoja,
Toloi kupata wana, ni furaha kwetu sote.

Ni furaha kwetu sote, tunamtukuza Mola,
Mungu Muweza wa yote, asante kujibu sala,
Tuzuie tusikwate, wewe huna kibadala,
Toloi kupata wana, ni hidaya kubwa hino,

Ni hidaya kubwa hino, Kiroboto naswifia,
Namwinua Mungu mno, tena namsujudia,
Katimizia maono, wale nilohurumia,
Toloi kupata wana, la ziada sina tena.

La ziada sina tena, ila nasaha hatima,
Toloi leeni wana, kwa ndia iliyo njema,
Wakamheshimu Bwana, isiwapate nakama,
Toloi kupata wana, shangwe Mulembe Ef Emu.

Ochieng’ O. Sylvester
Kiroboto Mpole”
Chuo Kikuu Cha Moi
Chepkoilel.






Kwaheri Mrono

Mpole nina kilio, kilio cha Kiswahili,
Silipati kimbilio, kulitia pigo hi9li,
Mauti faradhi ndio, bali hiki kikatili,
Kwaheri ndugu Mrono, mwalimu wa heba kubwa.

Twamshukuru Rabuka, kwa maishayo mwandani,
Sie tutakukumbuka, kwa kaziyo vitabuni,
Kukupeza ni hakika, sautiyo redioni,
Kwaheri ndugu Mrono, mwalimu wa heba kubwa.

Wapenzi wa Kiswahili, tumebaki vinywa wazi,
Kote metulia tuli, tangu lizame jahazi,
Mwenzetu kwa kwenda mbali, umetutia duwazi,
Kwaheri ndugu Mrono, mwalimu wa heba kubwa.

Bahari yetu si shwari, imechafuka watani,
Tangu uwe mhajiri, hatwoni chako kifani,
Twafazaika twakiri, hatutaki kuamini,
Kwaheri ndugu Mrono, mwalimu wa heba kubwa.

Kaketu wende salama, mikono yetu twapunga,
Wasalimie wa zama, akina Mwalimu Mbega,
Twakwombea kwa Karima, na dhiki atakutenga,
Kwaheri ndugu Mrono, mwalimu wa heba kubwa.

Kituoni nikifika, rambirambi nazituma,
Makiwa ndu’ watukuka, nayo familia nzima,
Haya mambo ya Rabuka, nayo mauko lazima,
Kwaheri ndugu Mrono, mwalimu wa heba kubwa.

Ochieng’ O. Sylvester
Kiroboto Mpole”
Chuo Kikuu Cha Moi
Chepkoilel.



No comments:

Post a Comment