Tuesday 18 September 2012

Chombo kikitia nanga


Mzee ni ukumbini, na tabu la ujanani,
Natia macho miwani, nimsomee Fulani,
Maisha ya duniani, wangi hawajui nini,
Chombo kikitia nanga, si mwisho wa usafiri.

Si mwisho wa usafiri, hata kama umefika,
Huishi kwenye bandari, kwenda zaidi tataka,
Ipe mgongo bahari, na uikabili njia,
Chombo kikitia nanga, teremka kwa makini.

Teremka kwa makini, uikague sehemu,
Jua lengo kuu nini, nakili kwa tarakimu,
Kama ndipo ubaini, lau sipo ufahamu,
Chombo kikitia nanga, yasubiri maelezo.

Yasubiri maelezo, usanze bure kuranda,
Yako kote matatizo, kokote unakokwenda,
Hayakeri maulizo, wangi mno mewalinda,
Chombo kikitia nanga, usanze kutoa mali.

Usanze kutoa mali, itatwaliwa haraka,
Ufikiri mara mbili, uhakiki umefika,
Wanolipuuza hili, huchekwa wanapotoka,
Chombo kkitia nanga, sikiza yao wazee.

Sikiza yao wazee, kama miye Kimpole,
Tukiteswa tutetee, radhi tulinazo tele,
Acha nende waombee, Mola awone milele,
Chombo kikitia nanga, umkumbuke Rabuka.

No comments:

Post a Comment